Kagera Yatengewa Hekta 58,000 Kwa Ajili Ya Viwanda
Na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa mikakati inayoendelea kutekelezwa na kuratibiwa katika Mkoa wa Kagera ni pamoja na kutenga maeneo ya uwekezaji yenye ukubwa wa hekta 58,000 kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo (Agro Processing Industries) hususani viwanda vya kusindika nyama, maziwa, asali, ndizi, miwa, kahawa na samaki.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, alipokua akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalaum Mhe. Halima Bulembo, aliyeuliza mkakati wa Serikali wa kuwa na miradi maalum ya kuondoa umasikini kwa Watu wa Kagera ambao ndio Mkoa pekee unaopakana na nchi nyingi zaidi za EAC na hivyo kuufanya kuwa Mkoa wa kimkakati kibiashara.
Alivitaja baadhi ya viwanda hivyo kuwa ni Kagera Fish Co. Ltd na Supreme Perch Ltd vinavyosindika minofu ya samaki, Kagera Sugar Co. Ltd na Amir Hamza Co. Ltd vinavyosindika miwa na kahawa, na Kiwanda cha Mayawa kinachosindika Mvinyo ya Rosella na juisi.
” Kampuni ya Josam imepatiwa eneo lenye ukubwa wa hekta 500 katika ranchi ya Kikulula na tayari imejenga bwawa kwa ajili ya kuvuna maji pamoja na kuanza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa wapatao 100 hadi sasa” aliongeza Dkt. Kijaji
Dkt. Kijaji alieleza kuwa mkakati wa kutekeleza miradi maalum ya kuondoa umasikini katika Mkoa wa Kagera imeainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021, Mpango Mkakati wa Mpango wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Mipango ya Mkoa wa Kagera kwa ujumla.
“ Miradi yote ya kiuchumi na kijamii inayotekelezwa na Serikali na Sekta Binafsi katika mkoa wa Kagera, na mikoa mingine ni kwa ajili ya kuondoa umaskini na kuboresha maisha ya wananchi”, alisema Dkt. Kijaji.
Aidha, aliainisha baadhi ya mikakati inayoendelea kutekelezwa na kuratibiwa na Serikali katika mkoa huo kuwa ni pamoja na kuimarisha usafiri wa majini kwa kukamilisha ujenzi wa meli kubwa itakayotoa huduma ya usafiri na usafirishaji kati ya Bukoba na Mwanza.
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya barabara kama vile barabara kwa kiwango cha lami ya Kyaka – Bugene (km 59.1), Kagoma – Lusahunga (Km. 154), Ushirombo – Lusahunga (Km. 50).
Alizitaja barabara nyngine zinazojengwa katika ukanda huo kuwa ni barabara ya Nyakanazi – Kibondo (km 50), ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 40 pamoja na barabara ya Kyamyorwa – Buzirayombo (km 120).
“Kitaanzishwa kiwanda cha kuchakata madini ya bati katika wilaya ya Kyerwa ifikapo Juni, 2021 ambapo Kampuni ya Tanzaplus Minerals na African Top Minerals ltd zimeonesha nia ya kuwekeza katika sekta hiyo na tayari zimeanza kuleta mitambo ya uchenjuaji” aliongeza Dkt. Kijaji
Aliutaja mradi mwingine wa sekta ya madini kuwa ni uendelezaji na uwekezaji wa madini ya Nikeli Kabanga katika Wilaya ya Ngara ifikapo Juni mwaka 2021.
Mbunge wa Ilolo Mhe. Venance Mwamoto, aliuliza mpango wa Serikali wa kukarabati barabara za mkoa wa Kagera kwakuwa una viwanda vingi ili viweze kufikika kwa urahisi na kurahisisha biashara ndani na nje ya nchi.
Akijibu swali la nyongeza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Atashasta Nditiye alisema kuwa Serikali imeshapeleka fedha katika mkoa huo na tayari imetoa tangazo la kutafuta Wakandarasi kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo.
Hakuna maoni