Jeshi La Polisi Mbeya Linawashikilia Watu 21 Kwa Tuhuma Mbalimbali Ikiwa Ni Pamoja Na Kufanya Shughuli Za Uganga Bila Kibali
KUPATIKANA NA MALI IDHANIWAYO YA WIZI.
Mnamo tarehe 23.03.2019 saa 14:39 mchana huko eneo na Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi walimkamata JOSEPH MGAYA [27] Mkazi wa Ilomba akiwa na Pikipiki MC 395 BYN aina ya Kinglion ambayo mtuhumiwa amekiri kuiiba Pikipiki hiyo huko Kijiji cha Lupatingatinga Wilaya ya Chunya. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.
KUFANYA SHUGHULI ZA UGANGA BILA KIBALI.
Mnamo tarehe 25.03.2019 saa 00:10 usiku huko katika Kitongoji cha Mapinduzi ‘B’ kilichopo katika Kijiji cha Idunda, Kata ya Itewe, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi walimkamata PASCHAL PATRICE [30] Mkazi wa Kijiji cha Idunda na wenzake 19 wakifanya shughuli ya uganga bila kibali.
Watuhumiwa wote wakiwemo wanawake 03 walikutwa wakiwa kwenye nyumba ya mtu aliyefahamika kwa jina moja la MWARABU mkazi wa Dar es salaam. Pia katika nyumba hiyo wamekutwa watu watatu wote wanaume waliokuwa wamekwenda kutibiwa hapo. Upekuzi umefanywa ndani ya nyumba hiyo na kufanikiwa kupata begi ambalo ndani yake likiwa na kibuyu kimoja, chupa mbili za plastiki zenye unga unaodhaniwa kuwa ni dawa za kienyeji, kikopo cha plastiki cha njano chenye unga unaodhaniwa kuwa dawa za kienyeji zinazotumiwa na waganga kutolea tiba pamoja na ngoma moja. Upelelezi unaendelea.
Gari aina ya FUSO lililokuwa likisafirisha magunia ya Mahindi kwenda nchini Malawi kwa njia ya magendo.
KUSAFIRISHA BIDHAA NJE YA NCHI BILA KIBALI.
Mnamo tarehe 24.03.2019 saa 12:15 mchana huko Kitongoji cha Mwambuluko, Kijiji cha Isaki, Kata ya Katumbasongwe, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa mbeya. Askari Polisi walikamata gari moja lenye namba T. 268 BNH aina ya Mitsubishi Fuso truck likiwa limebeba magunia yenye nafaka mahindi makavu yapatao magunia 88 mali ya mtu mmoja aitwaye DORIN KAONGA [35] Mmalawi, Mfanyabiashara na Mkazi wa Kalonga – Malawi na GLORY KAFWILA [32] Mmalawi, Mfanyabiashara na Mkazi wa Kalonga – Malawi.
Dereva wa gari hilo alikimbia kusikojulikana na msako mkali wa kumtafuta unaendelea. Gari hilo lilikua likielekea kivuko haramu cha Nyasa katika mto Songwe mpakani mwa nchi ya Tanzania na Malawi kwa ajili ya kuyavusha magunia hayo ya mahindi kwa mitumbwi kuelekea nchi hiyo jirani ya Malawi.
Gari hilo lililotumika kubeba magunia hayo ya mahindi ni mali ya mtu mmoja aitwaye SHABAN ADIL KAJUNI wa huko Wilaya ya Rungwe. Vielelezo gari hilo na magunia hayo ya mahindi vimekabidhiwa mamlaka ya mapato idara ya forodha Kasumulu na hatua zaidi za kisheria. Upelelezi unaendelea.
Hakuna maoni