Shambulio katika misikiti New Zealand: Watu 49 wameuawa katika shambulio la kigaidi katika mji wa Christchurch
Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda
Ardern anasema watu 49 wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa
vibaya baada ya kuzuka mashambulio katika misikiti miwili katika mji wa
Christchurch, huko New Zealand.
Waziri mkuu huyo amelitaja shambulio hilo kuwa mojawapo lililotanda 'kiza kikubwa' siku ya leo nchini humo.Wanaume watatu na mwanamke mmoja wamekamatwa, kamishna wa polisi Mike Bush anasema, lakini ameonya kwamba huenda washukiwa zaidi wapo.
Inaarifiwa kwamba washambuliaji hao hawakuwa kwenye orodha ya magaidi wanaosakwa lakini ni wazi kwamba wana itikadi kali.
Waziri mkuu wa Australia Scott Morrison amesema mojawapo ya waliokamatwa ni raia wa Australia.
Amemtaja mshukiwa wa shambulio hilo kuwa "gaidi mwenye itikadi kali za mrengo wa kulia".
Walioshuhudia mkasa huo wameambia vyombo vya habari kwamba walilazimika kutoroka kuokoa maisha yao na waliona watu walioanguka chini wanaovuja damu nje ya mskiti wa Al Noor.
Polisi inasisitiza kwamba hali bado haijaimarika na wamethibitisha pia kwamba "vilipuzi kadhaa vilivyofungwa kwenye gari vimeharibiwa".
Maafisa wameshauri misikiti yote katika mji huo ifungwe mpaka ilani itakapotolea, wakieleza kwamba hili lilikuwa shambulio la vurugu ambalo halikutarajiwa.
Mohan Ibrahim, ambaye alikuwa katika eneo hilo la msikiti wa Al Noor ameliambia gazeti la Herald: "Awali tuliona ni hitilafu za umeme lakini mara tu, watu wote wakaanza kutoroka.
"Bado rafiki zangu wamo ndani. Nahofia usalama wa maisha ya rafiki zangu
Bado haijulikani wazi nini kilichofanyika ndani ya misikti hiyo, taarifa mpaka sasa zimetoka kwa walioshuhudia mkasa na waliozungumza na vyombo vya habari.
Mashahidi wametaja kuona watu wakiwa wameanguka chini wanavuja damu.
Hakuna maoni