Kanisa la walevi Turkana kaskazini magharibi mwa Kenya
Kanisa la Full Combat Jerrycan ni
kanisa linalohudhuriwa na walevi katika kijiji cha California mjini
Lodwar, kaskazini mwa Kenya.
Kanisa hili ambalo ibada hufanyika
chini ya mti, waumini wake huhudhuria wakiwa walevi wa pombe za
kienyeji, inayojulikana kama Kaada kwa lugha ya Kiturkana.
Kanisa
hili lilianzishwa mwaka wa 2016 na waumini wake wote ni walevi kutoka
kwenye maduka ya kuuzia pombe za kienyeji katika soko la California.
Aidha
jina la kanisa hili limezua utata kwa kuwa waumini wake wanasisitiza
kuwa linajulikana kama Full Combat Jerrican huku mhubiri akisisitiza
kuwa ni Redeemed Gospel.
Mhubiri wa kanisa hilo Peter Ekatorot
anasema kwamba alianzisha kanisa hilo wakati ambapo kijiji hicho
kilijulikana sana kwa uhalifu.
"Tulianza na watu watatu wakati
ambapo eneo hili lilijulikana sana. Mahali ambapo wakora sugu waliishi,
walevi na mahali ambapo ugonjwa ulikuwa umekithiri sana, hata makanisa
mengi yaliogopa sana. Makanisa yalikuwa yanafurushwa, watu wanamwagiwa
pombe, wanatukanwa hadi ikawafanya wachungaji wengi kuogopa kuja hapa.
Mhubiri huyo anasema kuwa alifika huko baada ya Mungu kumtuma kuwahudumia 'watu wake'.
"Nilikuja
nikaongea na watu moja kwa moja, halafu Jumapili ya kwanza tulipoanza,
watu watatu tu pekee ndiyo walikuja. Wengine walikuwa tu wanaendelea na
shughuli zao".
Hata hivyo ni kazi ambayo ilimlazimu kuwa na uvumilivu.
"Wakati
tulipoanza wiki ya pili, ikawa sasa wakati tunapofanya ibada, wengine
wanapigana, wanafukuzana ndani ya kanisa lakini niliweza kuvumilia
nikijua ya kwamba Mungu huleta mtu mahali ambapo atakomaa".
Kanisa hili pia liko na waimbaji na Susan Akimat ni mmoja wa wanakwaya ambaye amepunguza ulevi baada ya kujiunga na kanisa hilo.
"Kwanza sisi tulikuwa walevi sana, lakini sasa tumebadilika kidogo. Hii kanisa imetusaidia, kuna wale tumebadilika kiasi, lakini wengine pia watabadilika tukiendelea. Saa zingine tunaamua kama wanakwaya kupanga nyimbo zile tutakazoimba. Tulimwambia pia mhubiri wetu atusaidie kushona sare za kwaya, ili tujulikane kama wanakwaya."
Kevin Erot ni mshirika wa kanisa hilo na anasema kwamba imemsaidia sana kumjenga kiroho na hata kumwezesha kupunguza ulevi.
Hakuna maoni