Boeing 737 Max: Kampuni ya Marekani inayotengeneza ndege iliyoanguka Ethiopia yasitisha matumizi ya ndege zote aina hiyo
Kampuni
ya Boeing Marekani inayotengeneza ndege iliyoanguka Ethiopia imesitisha
matumizi ya ndege zote aina hiyo baada ya wachunguzi kubaini ushahidi
mpya katika eneo ambako ndege ya Ethiopia Airlines ilianguka.
Kampuni hiyo ya Marekani imesema itasitisha usafiri wa ndege zote 371 zinazohudumu.
Shirika
linalosimamia usafiri wa anga Marekani FAA, limesema ushahidi mpya
pamoja na data mpya za satelaiti zimechangia uamuzi huo wa kupiga
marufuku kwa muda usafiri wa ndege hizo.
FAA awali lilisisitiza ndege ya Boeing 737 Max 8 ni salama wakati mataifa mengine yakipiga marufuku usafiri wa ndege hizo.
Ajali hiyo siku ya Jumapili mjini Addis Ababa ulisababisha vifo vya watu 157.
Ni
ajali ya pili kuwahi kushuhudiwa ya ndege hiyo chapa Max 8 katika miezi
mitano baada ya ajali nyingine nchini Indonesia mwaka jana Oktoba
iliosababisha vifo vya watu 189.
FAA lina kundi la maafisa
wanaochunguza mkasa huo katika eneo ambapo ajali ya shirika la ndege la
Ethiopia ilipotokea likishirikiana na bodi ya kitaifa ya usalama wa
safari.
Dan Elwell, kaimu msimamizi katika shirika hilo FAA,
amesema Jumatano: " Imebainika wazi kwa pande zote kwamba safari ya
ndege ya Ethiopia ilikaribiana na namna ilivyoshuhudiwa kwa ndege
iliyoanguka awali ya Lion Air ."
Ameongeza kwamba "ushahidi
tuliopata katika eneo, umefanya kuwa na uwezekano mkubwa kwamba hata
njia ya ndege ilikaribiana na ile ya Lion Air".
Rais
Donald Trump awali alitangaza kwamba shirika la FAA litatoa tangazo la
dharura kufuatia "taarifa mpya na ushahidi tuliopokea kutoka eneo la
mkasa na kutoka maeneo mengine kupitia malalamiko mengine tofauti".
Marekani
ni nchi ya hivi karibuni kusitisha usafiri wa ndege hiyo ya Boeing 737
Max yakiwemo mataifa mengine kama Uingereza, Umoja wa Ulaya, China India
na Australia ambayo yote yameamua kusitisha usafiri wa ndege hizo.
Hakuna maoni