DRC: Rais Felix Tshisekedi amewaachilia huru mamia ya wafungwa wa kisiasa
Hatua ya Rais Felix Tshisekedi wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwaachilia huru wafungwa 700 wa
kisiasa imeendelea kuzua mjadala kote nchini humo.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamempongeza rais Tshisekedi kwa kutimiza ahadi yake na kuwaachilia huru wafungwa hao.''Kuna matumaini makubwa katika utawala huu hasa katika suala la kuheshimu haki za binadamu'', mmoja wa wanaharakati aliiambia BBC.
Kwa mujibu wa idara magereza nchini DRC wafungwa hao wanasubiri barua rasmi ya serikali kabla ya kuruhusiwa kutoka gerezani.
''Huu ni mchakato ambao unaweza kuchukuwa siku moja au zaidi, sidhani kama leo wataachiliwa huru na kurejea makwao'', Mmoja wa maafisa wa magereza ambaye hakutaja jina lake litajwe aliiambia BBC.
Mkurugenzi wa baraza la mawaziri, Vital Kamerhe, alitangaza hatua hiyo ya rais kwa taifa usiku wa Jumatano.
Miongoni mwa wafungwa waliyoachiliwa huru ni Firmin Yangambi, wakili aliyekamatwa mwaka 2009 na kuhukumiwa kifo mwaka mmoja baadae.
Wakili huyo alituhumiwa kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria na jaribio la kupanga maandamano dhidi ya serikali.
Mwingine ni Franck Diongo ambaye alikamatwa mwaka 2016 kwa tuhuma za kuzuilia mali ya walinzi watatu wa rais kwa kutumia amri ya mahakama.
Bwana Kamerhe pia alisema kuwa watu wote waliyokamatwa kwa kushiriki maandamano ya kupigania demokrasia kati ya mwaka 2015 na 2018 wataachiliwa huru.
Hatua ilipaswa kuchukuliwa mwaka 2015 kama sehemu ya mwafaka wa kisiasa uliyofikiwa chini ya usimamizi wa kanisa katoliki uliyopendekeza wafungwa wote wa kisiasa kuachiliwa huru kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi.
Katika mwafaka huo kanisa katoliki pia lilipendekeza wanasiasa wa nchi hiyo wanaoishi uhamishoni waruhusiwe kurudi nyumbani.
Hakuna maoni