Header Ads

ad728
  • Breaking News

    Masau Bwire: OCS Aridhiki Anastahili Pongezi


    Masau Kuliga Bwire
    OCS Aridhiki, wa kituo cha polisi, Tabata, Dar Es salaam, anastahili pongezi, ni mfano wa kuigwa, ana kasi inayoendana na Rais Magufuli.
    Asubuhi leo, March 17, 2019, nikalazimika kuwepo kituo cha Polisi Tabata, kufuatilia tukio la msichana mmoja aliyechomwa kisu cha paja, mbele yangu, kisa Kiberiti!

    Dada huyo, jana alimuazimisha jamaa mmoja kiberiti, hakumrudishia, leo alipomdai, jamaa akaona ni usumbufu na kudhalilishwa, akaja juu, akamshambulia kwa kipigo, kisha kamchoma kisu cha paja.

    Rais Magufuli.
    Asubuhi, saa 1 hivi, nikiwa kituo cha kuosha magari, Carwash, hapa Tabata Relini, ghafla kukazuka ugomvi jikoni, kati ya mdada, Ashirati na jikaka pandikizi, lililopanda kwenda hewani, kwa jina linalotambulika, Mwaikimba, ni la huko huko kwa akina ‘Mwa’, likimshambulia dada huyo, likitishia kumpiga kwa kipande cha tofali na kuni vilivyokuwepo jikoni hapo kwa ajili ya kuchoma nyama tayari kwa walaji mchana wa leo, hii ni baada ya kumtandika kofi lenye uzito mkubwa dada huyo mrembo!

    Hapo Carwash, pembezoni kuna banda la chakula na vinywaji, dada huyo uhudumu hapo.
    Jamaa, bila aibu, lilitwaa kisu kilichokuwepo jikoni hapo, kikisubiri kutumika kukatia nyama, na kumkita dada huyo katika paja lake la kulia!

    Mshefa baada ya hapo, akachukua mdogo mdogo, akapotelea kusiko julikana!
    Muda wote huo mimi nilisimama nikishangaa, nakudhani Mwaikimba anazozana na mwanaume mwenzake aliyetazamana naye, hivyo sikuwa na presha sana ya kutoa msaada, kumbe dogo alisimama kati, kumuokoa dada huyo na kipigo cha Mwaikimba!

    Baada ya Mwaikimba kutokomea, niliona watu wanamzunguka mrembo huyo kwa mshangao, nilijisogeza kujua kulikoni, loo, mrembo damu zinamchuruzika katika paja lake, la mguu wa kulia, huku vijana wakijaribu kumfunga tambala ili kuzuia mchuruziko huo wa damu kuendelea.

    Sikuwa na namna nyingine, nilisitisha gari kuoshwa nikambeba hadi kituo cha polisi Tabata tukaandikiwa PF 3, kisha kituo cha Afya Tabata, ambapo alipata huduma ya matibabu, akashonwa nyuzi 5.

    Kabla ya hapo niliwasiliana na Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata, aliyenipa ushirikiano mzuri sana katika kumpatia huduma majeruhi na namna ya kumtafuta na kumkamata aliyemjeruhi.

    “Waambie walioko hapo, wambebe kwa gari au bodaboda, wampeleke hapo kituoni, aandikiwe pf 3, wampeleke Hospitali, gharama zitakazokuwepo, nitazilipa” alisema OCS huyo, mwanamke wa kituo cha polisi Tabata.

    Baada ya matibabu, nilimrudisha majeruhi kituo cha polisi ili akaandike maelezo na kufunguliwa kesi kama alivyoelekeza OCS wa kituo hicho, akisisitiza nasi mashuhuda wa tukio tutoe maelezo yetu kabisa ili shitaka hilo lishughulikiwe kwa haraka, mtuhumiwa akamatwe, apelekwe mahakamani haraka iwezekanavyo.

    “Wengine ondokeni, abaki huyu aliyejeruhiwa, niandike maelezo yake, maelezo ya mashahidi yatachukuliwa upelelezi ukianza”, alisema Sajenti mmoja aliyekuwepo kaunta kituoni hapo.
    Nikiwa njiani kuendelea na mihanjo yangu, baada ya kuondolewa kituoni hapo na Sajenti huyo, OCS alinipigia akitaka kujua nini kinaendelea….

    “Nimeondoka, nimemuacha majeruhi akiandika maelezo, sisi mashuhuda tumeambiwa maelezo yetu yatachukuliwa upelelezi utakapoanza”, nilimjibu OCS, mwana mama aitwaye Aridhiki.

    “Haiwezekani, tunahitaji mambo haya yaende haraka, hatua za haraka zichukuliwe, kuna ugumu gani kuandika maelezo ya mashahidi, nakuomba hurudi kituoni, nawapigia sasa hivi, ukaandike maelezo, tunahitaji tufanye kazi kwa haraka na kwa wakati, tusiweke ugumu panapowezekana”, alisema OCS Aridhiki.

    OCS Aridhiki alinielekeza nikifika kituoni, nimuone Sajenti God, ili anipe askari, CID Said twende naye eneo la tukio, akalikague na kuanza hatua za upelelezi.

    Nilipofika kituoni, nilikuta kila kitu kiko tayari, CID Said amejipanga, tayari kwenda eneo la tukio, nilimchukua hadi eneo la tukio na kufanya ukaguzi.

    Hakuna maoni

    Post Top Ad

    ad728

    Post Bottom Ad

    ad728