Kimbunga Kenneth: Mamlaka za Hali ya Hewa Msumbiji, Tanzania zatoa tathmini
Kumezuka hofu ya kimbunga kwenye upwa wa magharibi wa Bahari ya Hindi hususan katika nchi za Msumbiji na Tanzania.
Mtandao
uliobobea kwenye masuala ya hali ya hewa wa AccuWeather wa nchini
Marekani umeripoti kuwa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa katika bahari
ya Hindi huenda ukapelekea kutokea Kimbunga kitakachopewa jina la Kenneth. Iwapo kimbunga hicho kitatokea, kinatazamiwa kuathiri maeneo ya kuanzia Lindi kusini mwa Tanzania mpaka Pemba kaskazini mwa Msumbiji.
Mtandao huo pia umebainisha kuwa mgandamizo huo wa baharini unaweza kupoteza makali na kimbunga kisitokee, ila badala yake mvua kubwa zinaweza kutokea na kuathiri maeneo hayo.
"Mvua kali zinazoweza kusababisha mafuriko na mmomonyoko wa udongo katika maeneo kama Masasi na Tunduru nchini Tanzania, pia Marrupu na Montepuez kwa upande wa Msumbiji," imeeleza taarifa ta AccuWeather.
Mamlaka za Msumbiji zatangaza tahadhari
Ikiwa mwezi mmoja umepita tangu Msumbiji ilipopigwa na kimbunga Idai, mamlaka za nchi hiyo zimetangaza tahadhari ya uwezekano wa kutokea kimbunga kingine baadae wiki hii.
"Tutaendelea kufuatilia namna ambayo mfumo wa hali hiyo ya hewa unavyoendelea kuibuka na kujipanga kadri inavyotakiwa," Msemaji wa Taasisi ya Kupambana na Majanga wa nchi hiyo Paulo Tomás anaripotiwa kutoa kauli hiyo kwenye kikao kilichowashirikisha wataalamu kutoka idara za hali ya hewa, afya na ulinzi wa chakula za serikali ya Msumbiji.
Machi 14, baadhi ya maeneo ya Msumbiji, Malawi na Zimbabwe yalikumbwa na kimbunga Idai.
Kwa mujibu wa Kamati ya Dharura ya Majanga ya Uingereza watu 960 walipoteza maisha kutokana na athari za kimbunga hicho. Watu milioni tatu kwenye nchi hizo bado wanahitaji misaada ya kibinaadamu kama chakula, dawa, malazi na makazi.
'Haujafikia kiwango cha kimbunga'
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetoa taarifa kwa umma Jumatatu Aprili 22, kuhusiana na hali hiyo kwenye bahari ya Hindi, na kusema mifumo ya hali ya hewa inaonesha mgandamizo mdogo wa hewa katika eneo la kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.
"Mgandamizo huo haujafikia kiwango cha kimbunga kamili na upo mbali na pwani ya nchi yetu kwa sasa. Inatarajiwa mgandamizo huo utaimarika zaidi katika kipindi kifupi na kutawala mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa nchini mwetu," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mamlaka hiyo pia imetoa utabiri wa hali ya hewa kwa siku tano kati ya Aprili 22 mpaka Aprili 26.
Utabiri huo unatoa tahadhari kuwa siku ya Ijumaa, Aprili 26 kunategemewa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa baharini katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi na Mtwara.
"Tafadhali chukua hatua, uwezekano wa kutoke ni mkubwa na kiwango cha athari zinazoweza kutokea ni mkubwa," taarifa hiyo ya (TMA).
Kwa mujibu wa Meneja wa Utabiri wa Hali ya Hewa wa Kimataifa wa AccuWeather, kimbunga Kenneth kinatarajiwa kuzikumba Tanzania na Msumbiji Alhamisi usiku ama mapema Ijumaa wiki hii.
Hakuna maoni