'Kiongozi wa mapinduzi' Amhara, Ethiopia auawa na polisi
Kiongozi wa jeshi anayeshukiwa kuongoza jaribio la mapinduzi siku ya Jumamosi katika eneo la Amhara nchini Ethiopia, ameuawa na polisi, vyombo vya habari vya taifa vinaripoti.
Brigedia Jenerali Asaminew Tsige aliuwa nje kidogo ya makao makuu ya jimbo la Amhara, mji wa Bahir Dar, ripoti zinaeleza.
Mkuu wa jeshi, Jenerali Seare Mekonnen pamoja na maaafisa wengine wanne waliuawa wakati wakizuia mapinduzi hayo, maafisa wameeleza.
Waziri Mkuu Abiy Ahmed ametoa wito kwa raia wa Ethiopia kuungana dhidi ya nguvu za ''kishetani'' zenye nia ya kuigawa nchi yao.
Bendera zinapepea nusu mlingoti baada ya serikali kutangaza kuwa siku ya maombolezo.
Jenerali Saare na Gavana wa Amhara, bwana Ambachew Mekonnen ambaye pia aliuawa Jumamosi, walikuwa wakionekana kama washirika wakubwa wa Waziri Mkuu Abiy.
Vikosi vinavyounga mkono serikali vimepelekwa makao makuu ya mji wa Bahir Dar, pamoja na mji mkuu wa nchi Addis Ababa.
Mwasiliano ya intaneti yamezimwa nchi nzima, ikiwa ni siku chache tu toka mawasiliano hayo yaliporejeshwa baada ya kukatwa pasi na kutolewa sababu kwa wiki nzima.
Serikali ya Marekani imetahadharisha wafanyakazi wake mjini Addis Ababa kubaki majumbani.
Mapigano yameikumba Amhara na maeneo mengine ya Ethiopia miaka ya hivi karibuni.
Tangu kuchaguliwa kwake mwaka jana, Bwana Abiy amekuwa na nia ya kumaliza mivutano ya kisiasa kwa kuwaacha huru wafungwa wa kisiasa, kuondoa marufuku dhidi ya vyama vya siasa na kuwashtaki maafisa wanaoshutumiwa kukiuka haki za binaadamu.
Ethiopia ni nchi ya pili yenye watu wengi barani Afrika (baada ya Nigeria), ikiwa na watu milioni 102.5 kutoka kwa zaidi ya makabila 80.
Ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi , lakini idadi kubwa ya vijana nchini Ethiopia hawana ajira.
Brigedia Jenerali Asaminew Tsige, alikuwa ni mkuu wa usalama wa jimbo la Amhara.
Alikuwa ni miongoni mwa maafisa wa juu wa jeshi walioachiwa huru mwanzoni mwa mwaka jana baada ya serikali iliyopita kuwaachia wafungwa wa kisiasa kutokana na msukumo kutoka kwa umma.
Jenerali huyo alikuwa gerezani kwa miaka tisa akishutumiwa kupaga mapinduzi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Uingereza, la Reuters, maafisa wa juu wa Amhara walifanya mkutano siku ya Jumamosi kujadili majaribio ya jenerali ya kuwasajili wanamgambo.
Brigedia Jenerali Asaminew kwa wazi kabisa aliwashauri watu wa Amhara mwezi huu kujihami kwa silaha, katika video iliyosambaa kwenye mtandao wa Facebook na kushuhudiwa na mwanahabari wa Reuters.
Hakuna maoni