Waziri wa Kilimo: Machi 31 malipo ya wakulima wa Korosho yatakuwa yamekamilika
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Lindi
Serikali
imewahakikishia wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo
na Maji kuwa kufikia tarehe 31 Machi 2019 wakulima wote watakuwa
wamelipwa fedha zao kwani uhakiki umekamilika kwa kiasi kikubwa.
Hakikisho
hilo mbele ya kamati hiyo limetolewa leo Tarehe 16 Machi 2019 na Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) katika ukumbi wa mikutano kwenye
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi wakati akitoa ufafanuzi katika mkutano
uliowakutanisha wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wake
Dkt Christine Ishengoma, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Naibu Katibu Mkuu wizara
ya Kilimo, wataalamu serikalini sambamba na wakulima.
"Kumekuwa
na urasimu mkubwa tangu kuanza kwa zoezi hili la uhakiki lakini sasa
tumeamua kama serikali kabla ya mwisho wa mwezi huu wa tatu wakulima
wote wawe wamelipwa malipo yao ili kuondoa adha wanazokumbana nazo"
alikaririwa Mhe Hasunga
Alisema
pamoja na kwamba malipo ni mchakato unaohitaji kupitia katika hatua
nyingi za mchakato ikiwemo uhakiki lakini kila jambo lenye mwanzo ni
lazima kuwa na ukomo.
Alisema
mpaka sasa Tani 222,684 zimekwisha kusanywa huku hadi kufikia tarehe 14
Machi 2019 tayari jumla ya Shilingi Bilioni 596.9 zimekwishalipwa kwa
wakulima kati ya Shilingi Bilioni 723
Katika
hatua nyingine Waziri Hasunga amewahakikishia wajumbe wa kamati ya
kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa pamoja na mchakato huo wa
malipo ya Korosho kuendelea lakini pia Wizara imepitia katika michakato
mbalimbali ya kumpata Mkurugenzi mpya wa Bodi ya Korosho ili kuendelea
na majukumu ya Bodi hiyo.
Kuhusu
wanaofanya biashara ya zao hilo kinyume na sheria maarufu kama Kangomba
Waziri Hasunga alisema kuwa tayari serikali imewabaini na wote
watachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumzia
Pembejeo feki Mhe Hasunga alisema kuwa tayari hatua zimeanza
kuchukuliwa kwa wafanyabiashara wote waliofanya hujuma kwa kuwauzia
wakulima Mbegu na mbolea feki ambapo hatua kali zimeanza kuchukuliwa
dhidi yao ikiwa ni pamoja na kutolipwa fedha wanazodai kwa kusambaza
Pembejeo hizo.
Katika
hatua nyingine Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameuagiza
uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa viuatilifu Vya Tropiki (TPRI) kutuma
wataalamu Mkoani Lindi ili kuchukua sampuli za viuatilifu kwa wakulima
na kuvipima ili kubaini kadhia ya usambazaji wa viuatilifu feki kwa
wakulima.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge Dkt Christine
Ishengoma (Mb) amemuagiza Waziri wa Kilimo kuhakikisha kuwa taarifa ya
malipo ya wakulima wote wa Korosho inafika bungeni tarehe 2 Aprili 2019.
Hakuna maoni